Jumatatu , 13th Aug , 2018

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ali amesema kuwa chama chake mpaka sasa kimeshatekeleza nusu ya Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 na kusisitiza kuwa kazi inayoendelea kufanywa na serikali ni kusogeza zaidi huduma kwa wanyonge na wavuja jasho.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ali akisisitiza jambo.

Bashiru amefunguka hayo leo Jumatatu Agosti 13, 2018 jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kumtambulisha aliyekuwa mbunge wa Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka ambaye leo amejiunga na CCM na kusema kuwa chama chake kina silaha kubwa nne.

Amezitaja shahaba hizo kuwa ni kupambana na umaskini wa wanyonge, kutengeneza nafasi nyingi za ajira hususani katika sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo na viwanda, kupambana na rushwa na ufisadi na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama ili taifa liendelee kuwa na amani.

Katika kipindi hiki chini ya Rais John Magufuli tuko nusu ya utekelezaji wa Ilani yetu na bado tuna nusu nyingine, na katika ilani hiyo tunazo shabaha kubwa nne, Chama chetu kimeendelea kujisahihisha pale yanapotokea makosa, lengo kuu ni kuhakikisha misingi ya Azimio la Arusha na Mapinduzi ya Zanzibar yanaimarishwa”, amesema Dkt. Bashiru.

Kujiuzulu kwa Mbunge huyo wa Liwale kunafikisha jumla ya wabunge watano (5) kutoka vyama vya upinzani kujiuzulu nafasi zao za ubunge na kuhamia CCM ambao kati yao kutoka CUF ni watatu na wawili kutoka CHADEMA.

Wimbi la viongozi na wanachama wa upinzani kutimkia CCM, lilianza kushamiri mwaka jana ambapo mpaka sasa jumla ya wanachama milioni mbili wameshajiunga na chama cha mapinduzi kuanzia Januari mwaka 2017 hadi sasa kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole.