Fahamu jiwe la Laizer lilivyopatikana

Jumatatu , 3rd Aug , 2020

Imeelezwa kuwa jiwe la tatu la Tanzanite lililonunuliwa na Serikali hii leo, lilipatikana wakati wa kuondoa Mwamba uliokaribia kuanguka ndani ya mashimo anayoyamiliki Bilionea Saniniu Laizer.

Bilionea Saniniu Laizer.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 3, 2020, na Waziri wa Madini Doto Biteko, wakati akizungumza na wananchi katika zoezi la makabidhiano ya Jiwe la Tanzanite lenye uzito wa Kg 6.371 kati ya Serikali na Bilionea huyo.

"Katika kuondoa Mwamba uliokaribia kuanguka ili zoezi la uchorongaji liweze kuendelea na ndipo kipande hicho cha Kg 6.371 kilipatikana, ambapo Serikali imeamua kipande hicho chenye thamani ya Bilioni 4.846 ikinunue na itapa mrabaha wa Milioni 290", amesema Waziri Biteko.

Kwa upande wake Bilionea Laizer amesema kuwa wao kama wachimbaji wadogo wadogo wa madini, wameridhishwa na bei ya Serikali, kwa sababu haina longolongo na kuwaomba Watanzania wamchague Rais Magufuli.

"Nina uhakika ninaweza kutoa Mawe makubwa zaidi ya haya, tunaiomba Serikali iendelee kukata kodi kwa sababu inasaidia maendeleo, upande wetu Umasaini kila mtu anachota maji kwenye nyumba yake, Punda wamepumzika , Magufuli ni mwema kila mtu amchague popote alipo, tumempata Mfalme".