Jumanne , 28th Feb , 2023

Familia moja katika mtaa wa Mkunguni A kata ya Hananasifu manispaa ya Kinondoni imejikuta ikilala nje kwa zaidi ya siku 15 baada ya kutupiwa vyombo nje kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mgogoro wa kifamilia unaotokana na kugombania mali kati ya mjukuu na bibi ambaye ndiye alikuwa akiishi hapo

Akizungumza na EATV bibi huyo aliyefahamika kwa jina la Asha Ramadhani amesema nyumba hiyo amekuwa akiishi na mume wake kwa zaidi ya miaka 40 pamoja na watoto wake aliozaa na mume wake huku akieleza kuwa ana vielelezo vyote vya umiliki wa nyumba hiyo lakini ameshangazwa na mmoja wa wajukuu zake kumtaka bibi huyo aondoke katika nyumba hiyo

Kwa upande wake mjumbe wa serikali ya mtaa huo Rashid Salum amesema kutupiwa nje vyombo kwa familia hiyo kumefanyika kimakosa kwani notisi iliyowafikia ilikuwa na maelekezo ya nyumba namba 42 iliyopo mtaa wa Kawawa ambao sio mtaa huo ni mtaa mwingine tofauti na huo

Naye mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mkunguni A Said Juma Kidae akizungumzia sakata hilo ameiomba serikali kuingilia kati na sheria ifuate mkondo wake ili kila mmoja aweze kupata haki zake kutokana na bibi huyo kuendelea kuteseka kwa kulala nje zaidi ya siku 15 sasa