Jumatano , 27th Jul , 2022

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomoni Mwangamilo, amewaonya baadhi ya wamiliki na madereva wa mabasi yaendayo mikoani kuacha mara moja, tabia ya kushabikia mwendokasi kwani umekuwa ndiyo chanzo cha kupoteza maisha ya watu na atakayekamatwa atashughulikiwa kweli.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomoni Mwangamilo

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 27, 2022, wakati akiongea na madereva wa mabasi yaendayo mikoani katika stand kuu ya mabasi jijini Arusha, na kusema zipo taarifa kutoka kwa wananchi wema kuwa kuna baadhi ya wamiliki wanao washawishi madereva kwenda mwendo kasi na madereva hao kuyaendesha magari hayo kasi.

"Fimbo ya mbali ya kwetu polisi inaua Nyoka, kuna wamiliki wa mabasi wanashabikia mwendo, mtupe taarifa tutamfikia, na tutakachomfanya yeye ndiyo ataeleza tumemfanya nini, ajali zinaharibu system nzima za maisha ya watu, watu wamechoka kulia na kusononeka, nitakayemkamata nitamshughulikia zaidi ya kawaida," amesema SP Mwangamilo

SP Mwangamilo akawasisitiza madereva kuhakikisha wanafuata miiko ya uendeshaji na sheria za barabarani.