Jumapili , 28th Feb , 2016

Serikali imezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wananchi wote wanaishi katika maeneo salama katika kipindi hiki cha mvua ili kuwahepusha na kukumbwa na maafa pindi zinaponyesha mvua kubwa zinazosababisha mafuriko.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.KasSim Majaliwa

Agizo hilo limetolewa jana mkoani Mtwara na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.KasSim Majaliwa alipokuwa akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa, na kusema kuwa kwamujibu wa taarifa za watabiri wa hali ya hewa ni kwamba bado mvua zitakuwa nyingi na kubwa zaidi katika kipindi cha mwezi Machi mwaka huu.

Amesema serikali inawapa pole wote waliokumbwa na maafa hayo huku ikijitahidi kutoa misaada kwa waathirika kwa kadri inavyowezekana ili kupunguza ugumu wa maisha uliosababishwa na janga hilo.

Awali mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akitoa taarifa ya maafa hayo alisema jumla ya kaya 2177 na mashamba 5200 yaliharibiwa na mafuriko, huku kukiwa na vifo vya watu Tisa ambavyo vilisababishwa na Radi kali ambazo zilipiga wakati wa mvua na upotevu wa mali zenye thamani ya sh. Bilioni 1.8.