Jumatatu , 28th Mar , 2016

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mstaafu Dkt. Samson Mushemba amesema kwamba 'hapa ni kazi tu' katika kutenda mambo mema katika jamii ili kuashiria ufufuko wa kweli wa Yesu Kristo katika maisha kwa kuishi maisha yenye ushuhuda.

Baba Askofu Mushemba ameyasema hayo katika ibada ya Jumapili ibada ya Pasaka ya kukumbuka ufufuko wa Yesu Kristo katika usharika wa Kijitonyama Jijini Dar es salaam.

''Tunapokumbuka ufufuko wa Yesu Kristo iwe ni hapa kazi tu katika kuwaona wagonjwa kuwa na upendo baina yetu ndani ya jamii na kufanya mambo yenye manufaa kwa Taifa''

Akizungumza na waumini walioshiriki ibada hiyo Mchungaji wa Usharika wa Kijitonyama ambaye pia ni Mkuu wa Jimbo Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Anta Muro naye amewataka waumini kuwa na moyo wa ukarimu katika kusaidia watu wenye uhitaji maalumu katika jamiii.

Aidha kwaya mbalimbali ikiwemo kwaya toka usharika wa Shelui Mkoani Singida na kwaya za Usharika wa Kijitonyama zimeongoza ibada hiyo kwa kutoa ujumbe unaokumbusha umuhimu wa siku ya Pasaka na kuwasihi waumini kupenda kumtumikia Mungu.