Jumatatu , 27th Jul , 2015

Serikali imesisitiza kuwa haitaweza kupunguza ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini kutoka asilimia 25 hadi 10 kwa kuwa hayo yalikuwa ni makubaliano ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Waziri wa Fedha Saada Mkuya akizungumza jambo katika moja ya makongamano

Akizungumza jana jijini Dar es salaam waziri wa Fedha Bi. Saada Mkuya amesema serikali ya Tanzania iliiomba EAC, Kupunguza kodi kufikia asilimia 10 kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi tu kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam.

Bi. Saada amesema waliwekewa makubaliano ya hadi mwezi Juni na baada ya kipindi hicho kumalizika hakuna namna yoyote ambayo serikali inaweza kufanya ili kupunguza kodi hiyo kwa kuwa ni makubaliano ya EAC, na sio Serikali.

Aidha Waziri wa Fedha alikanusha madai ya kuwa kuna msamaha wa ushuru kwa waingizaji malori nchini na kusisitiza kuwa hakuna msamaha kwa watu hao bali serikali imefuta ushuru kwa viwanda vya ndani vinavyounganisha Malori hayo.