Jumamosi , 30th Jan , 2021

Rais Dkt. John Magufuli amemuagiza Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima, kuhakikisha anawafuatilia madaktari walioacha kazi katika hospitali ya rufaa mkoa wa Tabora kwa sababu ya maslahi na kuhamia hospitali binafsi na ikiwezekana afungiwe yeye pamoja hospitali aliyoikimbilia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 30, 2021, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la magonjwa ya dharura katika hospitali hiyo na kwamba haiwezekani serikali ipoteze pesa kwa ajili ya kusomesha madakatari na wao badala ya kuwatumikia wananchi wanaanza kuwa wabinafsi kwa kutaka maslahi makubwa.

"Mfuatilie huyo daktari aliyekimbia hapa, uifuatilie na hiyo hospitali ikiwezekana tunamfungia huyo daktari na tunaifungia na hiyo hospitali aliyoenda kutibia ili watu waanze kujifunza kwamba wizara ya afya siyo ya kuchezea tu, unamsomesha mtu kwa fedha za watanzania halafu anasema maslahi madogo", amesema Rais Magufuli.

Aidha Rais Dkt. Magufuli, "Madaktari wote wanapata mkopo kwa asilimia 100, unasoma pale kwa miaka mitano ukishatoka pale unasema maslahi madogo, si ungekimbia wakati unasoma hela yetu umekula halafu unasema maslahi madogo, nia ya serikali ni kuboresha maslahi lakini unaanza na kimoja, unaboresha maslahi wakati huna majengo wala vifaa vya kutosha".