Jumatano , 14th Nov , 2018

Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kufungwa kwa dirisha la kupokelewa na kupewa dhamana ya uwakilishi kupitia tiketi ya CCM kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine, mpaka sasa ni wabunge tisa pekee ndio wamejiuzulu.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Wabunge hao waliojiuzulu nafasi hiyo na wengine kufanikiwa kutetea nafasi zao kwa mara nyingine kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), saba kati yao ni kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) huku wawili wakitokea Chama cha Wananchi (CUF).

Wabunge hao kutoka CHADEMA ni; Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli), Chacha Marwa Ryoba (Serengeti),Godwin Moleli (Siha), James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati) na Joseph Mkundi (Ukerewe) huku upande wa CUF ni Maulid Mtulia (Kinondoni) na Zuberi Kachauka (Liwale . 

Chaguzi hizo za marudio zilipelekea upinzani kususia kuendelea kushiriki mara baada ya kupoteza majimbo yao mfululizo, ambapo CHADEMA kupitia mwenyekiti wake wa chama, Freeman Mbowe kilitangaza kujiondoa rasmi kushiriki chaguzi ndogo zote zilizotangazwa kufanyika na chaguzi zozote zitakazofuata zinazosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa madai kwamba tume hiyo inafanya kazi kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi.

Na baadaye CCM, kupitia kikao cha kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Chama hicho kilichokaa Oktoba 30, kilitangaza tarehe 15 Novemba kuwa ndio tarehe ya mwisho kwa Chama hicho kuwapokea maombi ya wenye nia ya kujiunga na Chama hicho na kupewa dhamana ya uwakilishi kupitia tiketi ya CCM kwa wabunge na madiwani kutoka vyama vingine.

Na kuongeza kuwa baada ya tarehe hiyo hakuna kiongozi yeyote atakayepewa nafasi ya kugombea uwakilishi wa Chama hicho katika uchaguzi wa marudio badala yake watakuwa wanachama wa kawaida