
Kada wa CCM Haider Hussein Gulamal, na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu
Kwa mujibu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Singida, kesi hiyo imetupiliwa mbali baada ya mashahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuwa na maelezo yanayofanana.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Consolata Singano ambapo amesema amezingatia ushahidi wa mashahidi 9 wa upande wa Jamuhuri waliofika mahakamani hapo ambapo hakuna ushahidi unaomgusa Gulamali moja kwa moja.
Amesema katika ushahidi wao kila shahidi ametaja rangi tofauti ambapo mmoja ametaja Kaki, mwingine nyeupe, huku wa mwisho akitaja rangi ya Brown jambo ambalo mahakama imeshindwa kuelewa bahasha ipi ilibeba fedha.
Pia amesema hata hatua za ukamataji hazikuainishwa vizuri kwani hakuna mahali palipoonesha pesa ziliwahi kutaifishwa hadi zilipofikishwa mahakamani, pia namna zilivyotunzwa mpaka kufikishwa kama ushahidi.
Katika kesi hiyo, miongoni mwa mashahidi ni Ofisa Usalama Mkoa wa Singida, Kiseo Nzowa anayedaiwa kupewa rushwa hiyo ambapo amedai anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Shahidi huyo amedai kuwa Gulamali alimpa Sh.Mil 2 ili amsaidie kupitisha jina lake kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Singida Kaskazini na kwamba yeye hakuwa Mjumbe Kamati ya Siasa Wilaya.
www.eatv.tv imejaribu kumtafuta Gulamali ili kujua namna alivyopokea hukumu ya kesi hiyo lakini namba yake haikupatikana.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Lazaro Nyalandu alijiuzulu kwa kile alichokidai kuwa ni kukosekana kwa demokrasia ambapo ilipelekea CCM kuitisha tena kura za maoni kwa ajili ya kumpata mgombea ubunge wa Jimbo hilo, Justine Monko ambaye hatimaye alifanikiwa kushinda kiti hicho.