
Hii inafuatia ripoti ya pamoja ya wanahistoria wa Cameroon na Ufaransa iliyochunguza ukandamizaji wa Ufaransa wa harakati za uhuru kutoka 1945 hadi 1971.
Katika barua kwa Rais wa Cameroon Paul Biya iliyotangazwa kwa umma siku ya Jumanne, Macron alisema ripoti hiyo ilionyesha wazi "vita vilikuwa vimetokea nchini Cameroon, ambapo mamlaka ya kikoloni na jeshi la Ufaransa walifanya vurugu za ukandamizaji za aina kadhaa katika baadhi ya maeneo ya nchi".
Lakini Macron hakuomba msamaha wazi kwa ukatili uliofanywa na wanajeshi wa Ufaransa katika koloni lake la zamani, ambalo lilipata uhuru mnamo 1960.
Kiongozi huyo wa Ufaransa aliwataja vigogo wanne wa kupigania uhuru waliouawa wakati wa operesheni za kijeshi zilizoongozwa na vikosi vya Ufaransa, akiwemo Ruben Um Nyobe, kiongozi shupavu wa chama cha kupinga ukoloni cha UPC.
Ufaransa iliwalazimisha mamia kwa maelfu ya raia wa Cameroon kukimbilia katika kambi za kizuizini na kuwaunga mkono wanamgambo wakatili kukomesha mapambano ya uhuru, shirika la habari la AFP linanukuu ripoti hiyo ikisema.
Makumi ya maelfu ya watu waliuawa kati ya 1956 na 1961, ripoti ya wanahistoria ilisema.