JPM amuita Lijualikali, amsifia "umependeza"

Jumatatu , 29th Jun , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemkaribisha jukwaani Mbunge wa Kilombero aliyemaliza muda wake kupitia CHADEMA Peter Lijualikali na kumuambia kuwa kwa sasa tangu ahamie CCM ameanza kupendeza.

Mbunge wa Kilombero aliyemaliza muda wake Peter Lijualikali, na kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Julai 29, 2020, alipokuwa akiwakaribisha Wabunge wa Morogoro wakati akihutubia wananchi wa Kilosa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo ikiwemo hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mahandaki ya reli ya SGR.

"Nimefurahi kumuona Lijualikali, leo atakuwa Lijualibaridi, ebu njoo usalimie kidogo, salimu kidogo acha kusoma wewe piga nondo najua umehamia CCM umeanza na kupendeza" amesema Rais Magufuli.

Kwa upande Lijualikali amempongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi, "Mh Rais unafanya kazi kubwa sana na Watanzania ni mashahidi na hakuna dhambi yoyote ambayo umeifanya, kama kuna dhambi umeifanya ni kutujengea SGR, na kupeleka umeme kila Kijiji naamini hii si dhambi bali ni baraka ambayo Mungu ametupa kupitia wewe".