Jumatano , 25th Mar , 2015

Jukwaa la katiba nchini (JUKATA) limeitaka serikali iache mara moja kuiyumbisha tume ya uchaguzi NEC kwa kuilazimisha iendeshe kura ya maoni tarehe 30 Aprili 2015.

Jukwaa la katiba nchini (JUKATA) limeitaka serikali iache mara moja kuiyumbisha tume ya uchaguzi NEC kwa kuilazimisha iendeshe kura ya maoni tarehe 30 Aprili 2015, kwani kwa kufanya hivyo upo uwezekano mkubwa wa kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wadau wengi

JUKATA imesema hali inaweza kuwa hivyo kwa kuwa imeonekana wazi kuwa uandikishaji hauwezi kukamilisha kabla ya tarehe iliyopangwa ya kura ya maoni na kuiacha tume iwe huru kufanya kazi zake pamoja na kuipatia fedha kulingana na mahitaji ya NEC.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam afisa mipango wa JUKATA bwana Mchereli Machumbana ameongeza kuwa jambo la muhimu ni uwezeshaji wa elimu ya uraia na elimu ya mpiga kura ya kutosha ili watanzania wajue thamani ya kura yao na kuitumia haki yao kwa kujitambua muda utakapofika.

Kwa upande wake mbunge wa Wawi mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed amesema kuwa haoni matumaini yoyote kuhusiana na mchakato wa kura ya maoni na uandikishaji wapiga kura kama utaanza kutumika April 30.

Wakati huo huo mheshimiwa Rashid amesema kuwa Raisi wa Tanzania aharakishe kusaini mswada uliopitishwa Bungeni kuhusu utoaji misaada kipindi cha maafa na elimu zaidi itolewe namna yakujikinga na majanga na miundombinu inayojengwa izingatie ubora zaidi.