Jumatano , 18th Sep , 2019

Leo Septemba 18, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeendelea kusikiliza kesi ya Mwandishi wa Habari Erick Kabendera, anayekabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la Uhujumu uchumi, ambapo ameieleza Mahakama kuwa baada ya kufanyiwa vipimo amekutwa na matatizo ya mgongo.

Erick Kabendera

Kabendera amefikishwa Mahakamani hapo akiwa bado anatembea kwa kuchechemea na kuieleza mahakama hiyo kwamba, alipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa ajili ya vipimo na majibu ya vipimo hivyo yalionesha kuwa ana matatizo hayo.

Kabendera ameyabainisha hayo mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi Agustine Rwizile, baada ya Wakili mwandamizi wa Serikali Wankyo Simon, kueleza shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 01, 2019.

Kabendera alifikishwa mahakamani hapo  Agosti 5, 2019, akikabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha fedha zaidi ya Sh milioni 173.2.