Jumamosi , 2nd Mei , 2015

Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani Iringa wametakiwa kufanya vikao vya mara kwa mara na walimu na wadau mbalimbali wa elimu ili kupunguza madai yao kwa serikali.

Katibu tawala wa Mkoa wa Iringa Bi.Wamoja Ayubu.

Katibu tawala wa mkoa wa Iringa Bi. Wamoja Ayubu amesema hayo kwenye uchaguzi wa mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) mkoani Iringa ambapo amesema vikao vitasaidia kutatua matatizo yao kwa wakati.

Bi Wamoja amesema serikali inaendelea kufanya taratibu za kulipa madeni ya walimu ikiwemo ya kutolipwa mishahara kulingana na madaraja yao, gharama za uhamisho na malipo ya mafunzo mbalimbali.

Naye mwenyekiti mpya wa CWT mkoani Iringa Bw. Stanslaus Mhongole amewataka walimu kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na kamati tendaji ya mkoa ili kuleta maendeleo kwenye sekta ya elimu.

Hata hivyo, viongozi hao wamewakumbusha walimu walimu kufanya kazi kwa kufuata sheria za kazi yao na kuachana na mambo ya kisiasa hususani katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.