Jumatatu , 19th Dec , 2022

Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga ikiongozwa na Mwenyekiti wake Rajabu Abdurahman imekataa taarifa ya mganga mkuu wa wilaya ya Pangani Maulid Majala kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Ushongo pamoja na nyumba ya Muuguzi katika kata ya Mwera 

Inaelezwa kuwa licha ya kuongezewa  fedha na serikali shilingi Milion 150 kwa ajili ya kuukamilisha tangu  Februari  mwaka huu lakini mpaka sasa bado una sua sua. 

Kamati hiyo imemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya pamoja na mganga wa wilaya hiyo wajitafakari kwani serikali inaleta fedha kwa wakati na hivyo wanahitaji waone maendeleo kwa wakati na wala hawahitaji maneno mengine 

Hayo yamebainika wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea Zahanati hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na baadae serikali ikaongeza kiasi cha shilingi Million 150 kwa ajili ya kumalizia na kuanza kutoa huduma kwa wananchi lakini  taarifa iliyotolewa inakinzana na uhalisia wa maendeleo ya mradi yaliyopo kwa sasa. 

Aidha umaliziaji wa Zahanati hiyo unaenda sambamba na ujenzi wa nyumba ya wahudumu wa afya ambao bado haujaanza kutekelezwa hatua ambayo imemfanya mbunge wa jimbo hilo Jumaa Aweso kuongeza kiasi cha Shilingi Million 5 kwa ajili ya kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. 

Akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi huo mganga mkuu wa wilaya ya Pangani Maulid Majala amesema  kuwa kumekuwa na changamoto ya kumalizika kwa ujenzi huo kutokana na kuchelewa kwa muda wa kuomba kubadilisha matumizi ya fedha hadi kufikia sasa akiieleza  kamati  hiyo kuwa fedha zilizopo zilishahamishwa kutoka kwenye akaunti ya Zahanati hadi kwenye mradi jambo ambalo limeonekana sio la kweli.

 "Kumekuwa na changamoto ya kuchelewa kuanza kwa mradi huu kutokana na muda wa kuomba kubadilishia matumizi ya fedha na vifungu vya matumizi kulikopelekea fedha hizi kuvuka mwaka, fedha za mradi huu zilishahamishwa kutoka kwenye akaunti ya Zahanati kwaajili ya utekelezaji wa mradi" alisema Majala. 

Awali akizungumza mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii wa wilaya hiyo ambaye pia ni diwani Akida Boramimi alisema kuwa kamati yake ilifanya ziara ya kutemblea maendeleo  ya mradi huo na kutoa maagizo ambayo ni pamoja na kuhamisha fedha kwenda kwenye mradi , kusambaza vifaa vya ujenzi lakini jambo hilo halikutekelezeka kwa wakati.

 "Hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa nyumba ya Mganga mimi nilifanikiwa kufika hapa kwaajili kukagua baada ya kuona fedha hizi zimevuka mwaka, tulitoa maagizo ya kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya mkurugenzi kwenda kwenye akaunti ya mradi, tuliagiza wazabuni watafutwe na shughuli za kusambaza vifaa vya ujenzi na shughuli nyingine zianze lakini jambo hilo mpaka sasa halijatekelezeka" alisema Boramimi. 

Akizungumza na wananchi wa kata ya Mwera katika mkutano wa hazara Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Tanga Rajabu Abdulrahman amemtaka mkurugenzi wa halmashauri pamoja na mganga mkuu wa wilaya hiyo kujitafakari kufwatia kusua sua kwa mradi huo na kusema kuwa hwatokubali watendaji ambao wamekuwa hawawajibiki ipasavyo katika majukumu waliyopewa. 

"Zahanati ya Ushongo wananchi waliijenga kwa fedha zao wenyewe walizochanga kupitia serikali ya kijiji, ili weweze kupata huduma za afya karibu, zahanati ile haijakamilika, mbunge kaenda kutafuta fedha million 150 huu ndio mchakato wa kimaendeleo tunaotaka  lakini halmashauri wamezembea toka mwezi wa pili mpaka leo sisi kama chama cha mapinduzi hatuwezi kukubali, "

 "Tumetoa kauli mkurugenzi ajitafakari na mganga wa wilaya ajitafakari , na hizi ni salamu zote kwa mkoa wa Tanga , miradi yote ambayo serikali inaleta fedha kwa wakati tunahitaji tuone maendeleo kwa wakati wala hatuhitaji maneno mengine" alisema Abdulrahman.

Mbunge wa jimbo la Pangani ambaye pia ni waziri wa maji Jumaa Aweso alisema kuwa kuzorota kwa miradi mbalimbali ya serikali katika wilaya hiyo imekuwa ni kasumba ya muda mrefu sasa ifike mahali wahusika wanaosimamia miradi hiyo wachukuliwe hatua pale wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo.