Alhamisi , 26th Jan , 2023

Mfanyabiashara mkoani Mwanza Yusuph Kassim, ameuawa na watu wasiojulikana shambani kwake, katika Kijiji cha Chabula wilayani Magu, baada ya kuvamiwa na watu hao akiwa na kijana wake wa kazi ambaye yeye alifanikiwa kuwatoroka watu hao.

Yusuph Kassim, aliyeuawa

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Wilbroad Mutafungwa, amesema Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limedhamiria kufanya upelelezi wa kina ili kubaini chanzo cha mauaji ya mfanyabiashara huyo.

Kamanda Mutafungwa amesema tarehe 23 ya mwezi huu majira ya usiku mfanyabiashara huyo akiwa shambani kwake na kijana aliyekuwa anamsaidia kazi shambani hapo ghafla wakatokea watu hao na kuwavamia huku kijana huyo akiwatoroka watu hao na kumuacha mfanyabishara huyo hadi kesho yake aliporudi na kuukuta mwili wa mfanyabiashra huyo ukiwa umelala pembeni ya bwawa ukiwa na jeraha kubwa kichwani.

"Marehemu alikuwa anatembelea shamba lake akiwa pamoja na kijana wake wa kazi anayefanya kazi ya kuangalia mifugo, usiku akavamiwa na watu watatu wanaume waliokuwa wameficha sura zao na vitambaa, walimshambulia kichwani kwa kutumia kitu chenye ncha kali, kijana wake alifanikiwa kuwatoroka watu hao na kukimbia ufukweni na kujificha," amesema Kamanda Mutafungwa.

Aidha Kamanda Mutafungwa amesema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo polisi kwa kushirikiana na kitengo cha uchunguzi wa sayansi jinai walifika eneo la tukio na kuukagua mwili huo na kuuhifadhi katika hospitali ya wilaya ya Magu huku upelelezi wa tukio hilo ukiendelea hadi watuhumiwa watakapokamatwa.