Alhamisi , 11th Jun , 2020

Mbunge wa Kilombero Peter Lijualikali, amewataka Wabunge wote ambao wameitwa na TAKUKURU kwa ajili ya mahojiano, waseme ukweli na si kudanganya.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali.

Lijualikali ameyabainisha hayo leo Juni 11, 2020, mara baada ya kutoka kufanyiwa mahojiano na taasisi hiyo kufuatia tuhuma walizozitoa dhidi ya CHADEMA, kuwa walikuwa wanakatwa mishahara yao kila mwezi, ambapo Wabunge wa kuchaguliwa walikuwa wakikatwa laki 5, huku Wabunge wa Viti Maalum wao walikuwa wakikatwa Milion 1.5.

"Mahojiano yalikuwa mazuri na ya kirafiki, niwaombe wenzangu ambao wanakuja kwamba TAKUKURU imejipanga wana kila taarifa, yaani kama umejipanga kuja kudanganya, hauwezi kudanganya kabisa" amesema Lijualikali.

TAKUKURU Makao Makuu imesema kuwa itawahoji jumla ya Wabunge 69, pamoja na waliowahi kuwa Wabunge wa CHADEMA, ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi wa malalamiko dhidi ya matumizi ya fedha za chama zilizolalamikiwa na baadhi ya waliowahi kuwa Wabunge kupitia chama hicho.