Alhamisi , 27th Oct , 2022

Kaya 255 za vijiji vitatu vya Igeleke, Usokami na Kibengu vilivyopo halmasauri ya wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa zitaondolewa kwenye eneo la hifadhi ya Shamba la Sao Hill.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula

Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea na kukutana na wananchi wa  kijiji cha Kibengu kilichopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
 
Dkt Mabula amesema uamuzi unaofanywa kuhusiana na eneo hilo  una nia njema kwa mustakabali wa taifa na vizazi vijavyo kwa kuwa kaya hizo zimekuwa zikifanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwemo kilimo cha mazao ya kudumu na mazao ya msimu na kuharibu mazingira.

"Mhe Samia amesema hamtaondoka bure na uthamini itafanyika kwa yoyote aliyetimiza masharti na kwa kuwa kijiji kimeandikishwa maana yake mmekidhi vigezo vya kulipwa, na kila mlichowekeza katika eneo husika hakuna atakayedhurika" amesema Dk. Mabula.
 
Mkoa wa Iringa unahusisha vijiji/mitaa 15 yenye migogoro ya matumizi ya ardhi ambapo vijiji hivyo vimeainishwa katika sehemu kuu sita kulingana na aina ya mgogoro na uamuzi uliotolewa na Baraza la Mawaziri.