"Kazi sio Urais tu, mtarogana bure" - JPM

Jumanne , 30th Jun , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amewataka wana CCM wote wanaoenda kugombea katika nafasi mbalimbali wakawe wavumilivu na wasije wakasababisha kuvunja umoja wao, hasa katika kipindi hiki cha kampeni kwani watapoteza mwelekeo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Juni 30, 2020, Jijini Dodoma wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Mapinduzi, mara baada ya kurejesha fomu yake ya kuwania nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, na kutolea mfano wa namna ambavyo watia nia wa Urais Zanzibar, walivvyojitokeza kwa wingi na kupelekea kuanza kutoleana maneno.

"Niwaombe sana hasa wagombea wa CCM na Urais wa Zanzibar, wakawe waangalifu sana katika kunadi nafasi zao wasiumizane, tunawapa nafasi washindani wetu, kazi siyo Urais tu na ndiyo maana Wenyeviti wangu wa CCM wa Mikoa wote walikuwa na uwezo wa kuwa Marais lakini mkasema nenda wewe Magufuli, na kuna majimbo naambiwa watia nia wako hadi 25, mtarogana na kuumizana bure, atakayechaguliwa Mungu anamjua" amesema Rais Magufuli.

Zaidi ya wanachama Milioni 1 wa Chama cha Mapinduzi, wamejitokeza kumdhamini Mwenyekiti wao Rais Magufuli katika fomu za kuwania kupitishwa na chama hicho ili kugombea Urais katika uchaguzi ujao.