Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Ally Juma Makoa
Mhe. Makoa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua utekelezaji miradi ya fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi .
"Tunajua Wizara hii kupitia ilani ya CCM inatakiwa kuongeza idadi ya watalii ifikie milioni 5 ifikapo 2025 hivyo kwa kazi anazozifanya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kweli zinawavutia watalii wengi na tunaendelea kumuomba sana Mhe Rais azidi kuiangalia Wizara hii kwa sababu pato lake liko nje nje," amesema Mhe. Makoa.
Amesema Kamati imetembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kushuhudia ujenzi wa lango la kisasa la kuingilia ,nyumba za watumishi, viwanja vya ndege, miundombinu ya maji na ukarabati wa barabara na maegesho ya magari na kumshukuru Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuipatia Wizara hiyo fedha kiasi cha shilingi bilioni 90.2.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimeharakisha utekelezaji wa miradi ya kuendeleza utalii katika maeneo yaliyohifadhiwa.
"Wizara ya Maliasili na Utalii ilipata fedha kiasi cha shilingi bilioni 90.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyo ndani ya maeneo tunayoyahifadhi na fedha hizi zilikua zinatokana na changamoto ya UVIKO 19 ambapo Hifadhi ya Mkomazi ilinufaika na fedha kiasi Cha shilingi bilioni 4.3," amesema Naibu waziri Masanja.