Kesi ya Kabendera kutafutiwa Hakimu mwingine

Alhamisi , 7th Nov , 2019

Kesi inayomkabili Mwandishi wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera, imesogezwa mbele hadi Novemba 20, 2019, baada ya Hakimu Augustine Rwizile, aliyekuwa akiisikiliza kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, ambapo kwa sasa kesi hiyo inasubiri kupangiwa Hakimu mwingine.

Akizungumza mahakamani hapo leo Novemba 7, 2019, Wakili Mwandamizi wa Serikali Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Vicky Mwaikambo, amesema kuwa kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la utakatishaji wa fedha zaidi ya Shilingi milioni 173, uhujumu uchumi na ukwepaji wa kodi.

Kabendera alikamatwa nyumbani kwake Mbweni, Jijini Dar es Salaam, na watu waliodaiwa kuwa ni maafisa wa Polisi, Julai 29, 2019.