Jumatano , 12th Nov , 2025

Hii inafuatia uamuzi wa timu ya Majaji watatu wanaosikiliza kesi hii wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru kutoa wito kwa magereza kumfikisha Lissu mahakamani leo pamoja na  mashahidi wengine  ili kesi iweze kuendelea.

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu inatarajiwa kuendelea leo Novema 12 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam baada ya kuahirishwa mnamo Jumatatu ya Novemba 10, 2025 baada ya upande wa Jamhuri kuieleza mahakama kuwa mshtakiwa hatoweza kufika mahakamani kutokana na hali ya usalama katika jiji la Dar Es Salaam kutokuwa nzuri.

Hii inafuatia uamuzi wa timu ya Majaji watatu wanaosikiliza kesi hii wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru kutoa wito kwa magereza kumfikisha Lissu mahakamani leo pamoja na  mashahidi wengine  ili kesi iweze kuendelea.

Akizungumza kwa niaba ya upande wa Jamhuri kabla ya uamuzi wa mahakama kutolewa, Wakili Thawabu Issa aliieleza mahakama kuwa taarifa za usalama wa Lissu walipokea kutoka kwa Mkuu wa Magereza baada ya kumuuliza kwa nini mshtakiwa hajafikishwa mahakamani.

Siku hiyo pia jamhuri iliomba kesi kuahirishwa kwa siku 14 kutokana na mashahidi waliopaswa kutoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya kushindwa kusafiri kuja Dar es Salaam kwa sababu za kiusalama.

Lissu ambae anatimiza miezi saba gerezani toka April mwaka huu alipokamatwa, anajitetea mwenyewe baada ya kuomba katika Mahakama ya ukabidhi (Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu) ajitetee huku jopo la mawakili zaidi ya 30 lililokuwa lilikimtetea wakibaki kama washauri.