Jumanne , 5th Jul , 2022

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Athumani Amasi, amesema kwamba katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yaliyotolewa hii leo hakuna mtahiniwa aliyefanya vibaya kwani watahiniwa wote wamefaulu kwa asilimia 99.87.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) Athumani Amasi

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 5, 2022, visiwani Zanzibar wakati akitangaza matokeo ya watahiniwa hao.

"Taarifa ya shule 10 za mwisho sikuionesha, nimezibainisha tu zile zilizofanya vizuri zaidi katika zile zilizofanya vizuri, kwahiyo hakuna mtu wa mwisho na ufaulu hapa ni asilimia 99.87, kwa kidato cha sita shule zote zimefanya vizuri, ila ukiwa-rank lazima atapatikana tu ambaye amewazidi wenzake kidogo, ni sawa na kusema wamepata A zote lakini mwingine ana A ya 87 na mwingine ya 89," amesema Kaimu Katibu Mtendaji