Jumapili , 30th Apr , 2023

Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), limetangaza kuanza kwa mtihani wa marudio wa kidato cha nne kwa wanafunzi 337 ambao matokeo yao yalifutwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.
Wanafunzi hawa ni wale waliofanya mtihani mwaka 2022.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt Said Ally Mohamed

Katibu Mtendaji wa NECTA Dkt Said Ally Mohamed amesema uamuzi wa watahiniwa hao kurudia mtihani umetokana na uchunguzi kuonyesha zaidi ya asilimia 60 ya waliofanya udanganyifu hawakupanga wao.

"Asilimia 60 ya watahiniwa waliofanya udanganyifu chanzo chake kilitokana na mipango iliyopangwa na kuratibuwa na vituo husika kwa kushirikisha wamiliki wa shule, wakuu wa shule, walimu na wasimamizi wa mitihani," amesema Dkt. Mohamed .

Aprili 11, 2023 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa maelekezo kwa wanafunzi hao kuomba kurudia mtihani na baada ya ombi lao kukubaliwa mtihani huo utafanyika kuanzia Mei 2 hadi 15 mwaka huu.