Jumatano , 24th Dec , 2025

Katika taarifa yake Haftar ameonyesha hisia za majonzi makubwa akiitaja ajali hiyo kuwa ni msiba wa kusikitisha.

 Kiongozi wa makundi yenye silaha mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, ametuma ujumbe wa rambirambi jana Jumanne, Disemba 23 kufuatia kifo cha Kiongozi wa Jeshi la Libya, Mohammed al-Haddad, na wajumbe waliofuatana naye katika ajali ya ndege karibu na mji mkuu wa Uturuki, Ankara.

Katika taarifa yake Haftar ameonyesha hisia za majonzi makubwa akiitaja ajali hiyo kuwa ni msiba wa kusikitisha.

Wengine waliotuma salamu za rambirambi kwa familia za Haddad na wajumbe waliofuayana naye, pamoja na wenzake katika jeshi ni pamoja na Bunge la Wawakilishi lililoko Benghazi.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia vifo hivyo.

Katika taarifa yake ya awali, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya, amesema kuwa mabaki ya ndege binafsi ya aina ya Falcon 50, iliokuwa ikielekea mjini Tripoli kutoka Uwanja wa Ndege wa Esenboga, Ankara, yalipatikana baada ya kufuatiliwa na vyombo vya usalama vya Uturuki kilomita 2 kusini mwa kijiji cha Kesikkavak katika wilaya ya Haymana.

Yerlikaya alisema mawasiliano na ndege hiyo ya biashara yalipotea saa 20:52 saa za eneo (17:52 GMT) – takriban dakika 42 baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Ankara. Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.