Jumatano , 4th Mei , 2016

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Khamis Kigwangalla amesema atamwendeleza binti Getrude Clement ambaye alipata fursa ya kutoa mada kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Binti huyo ambaye anatoka katika jiji la Mwanza ambaye anasoma katika shule ya sekondari Mnarani Mwanza alipata wasaa wa kuongea kwenye mkutano huo kama mwakilishi wa watoto na vijana duniani mbele ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Kutokana na binti huyo kuonyesha uwezo wa hali ya juu ya kuweza kuwasilisha mada hasa kutetea kutetea watoto ameweza kumfanya Naibu Waziri Kigwangalla kuahidi kumuendeleza katika shule ya kisasa atakapomaliza elimu ya kidato cha nne ambapo kwa sasa yupo kidato cha tatu.

''Kwa kuthamini kipaji chake na mchango wake, na kutambua nafasi yangu kama Naibu Waziri kwenye Wizara inayosimamia mambo ya Watoto, na kama Mbunge na Mzazi wa mabinti, lakini zaidi kama mtu kutoka kwenye background ya maisha ya chini na ninayethamini mchango wa elimu kwenye maisha yangu, nimeamua kujitolea kumsomesha kidato cha tano na cha sita kwenye shule za kisasa. Taasisi yangu ya misaada ya kijamii ya Hamisi Kigwangalla Development Foundation itamlipia ada za masomo yake ya high school'' Amesema Naibu Waziri Kigwangalla kwenye ukurasa wa 'facebook'.

Aidha binti huyo pia ameweza kutoa hotuba kwa wabunge wanaotetea haki za watoto ambapo wazazi wa binti huyo mwenye umri wa miaka 16 wanafanya kazi ndogondogo za ujasiriamali.