Ijumaa , 1st Mei , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, leo ameongoza Watanzania kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani huku akiahidi kuongezeka kima cha chini cha mishahara kutoka 265,000 hadi kufikia 315,000, ikiwa uchumi utaimarika.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza,Rais Kikwete amezungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka waajiri kuendelea kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa wafanyakazi mahali pa kazi, kulipatia ufumbuzi tatizo la mifuko ya jamii, ushiriki wa wananchi katika kujiandikisha kupiga kura na malipo kwa madeni ya waalimu.

Katika hotuba hiyo Rais Kikwete amesema kuwa uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani utafanyika kama ulivyopangwa mwezi Oktoba mwaka huu na kushangazwa na baadhi ya kauli zinazoelezwa na baadhi ya watu kuwa ana mpango wa kuongeza muda wa kukaa madarakani.

Akijibu madai ya wafanyakazi, Rais Kikwete ameanza kwa kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 aliyokaa madarakani, ambapo moja ya mafanikio ni kuanzishwa kwa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi, ambao utatumika kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia wakiwa kazini.

Amesema mfuko huo utaanza kufanya kazi mwezi ujao na tayari mkurugenzi wake amekwisha teuliwa.
Kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara pamoja na kiwango cha kodi ya mapato katika mishahara, Rais Kikwete amesema kuwa serikali inaendelea kuyafanyia kazi, na huenda katika bajeti ijayo mambo hayo yakawezekana.

Aidha jijini Dar es Salaam, vijana wasio na ajira za kudumu wameiomba serikali kuweka jitihada katika kuboresha mitaala ambayo itawasaidia vijana kuwajengea uwezo wa kujiajiri punde wanapohitimu masomo.

Katika mahojiano na East Africa Televisheni, vijana hao wamesema serikali imekuwa ikishughulikia masuala ya kupanda kwa kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi kila mwaka lakini kumekuwa na jitihada ndogo za uboreshaji sekta ya ajira nchini na kutaka kuwepo na jitihada za kufufua viwanda na miradi iliyotaifishwa na wawekezaji ili kukuza ajira.

Aidha wamewashauri vijana wenzao kutumia taaluma zao pamoja kujiunga katika vikundi ili waweze kujiendeleza kwa kujiajiri huku waliopo katika mfumo wa ajira wakilalamikia makato makubwa ya kodi katika mishahara yao.