Ijumaa , 10th Jul , 2020

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimemsamehe aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana, aliyekuwa amesimamishwa baada ya kupewa adhabu ya kalipio la miezi 18, baada ya kukiuka maadili ya chama na kusema kuwa kuanzia sasa anakaribishwa kuendelea kushiriki na wanachama wenzake.

Kushoto ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, katikati ni Rais Dkt Magufuli na kulia ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana.

Rai na msamaha huo umetolewa leo Julai 10, 2020, na Mwenyekiti wa chama hicho Dkt Magufuli, wakati chama hicho kikiendelea na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama ikiwemo uchaguzi wa kupata jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa ajili ya kugombea Urais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ndugu yetu huyu aliomba radhi hadharani ni kitendo kigumu sana kwa watu wa kawaida kukifanya, mimi alinigusa sana,nina uhakika hata ninyi Wajumbe iliwagusa sana, alikuwa amepewa adhabu ya kalipio la miezi 18, na hakukataa na mpaka sasa ametumikia miezi mitano sasa, niliona ndugu zangu niwaombe kama itawezekana tumsamehe" aliomba Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli akimzungumzia aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe amesema kuwa, "Yule mwingine ambaye sitaki kumtaja jina, yule ameshaondoka moja kwa moja adhabu ile si mmeikubali ya kumfukuza moja kwa moja?".