Ijumaa , 17th Oct , 2025

Kiongozi wa mapinduzi wa Madagascar, Kanali Michael Randrianirina ameapishwa kuwa rais kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana ambayo yalimlazimisha Rais aliyekuwepo madarakani Andry Rajoelina kulikimbia taifa hilo.

Katika hafla iliyofanyika katika Mahakama ya Juu ya Katiba mjini Antananarivo, Kanali Michael Randrianirina amekula kiapo chake akisema

Atatimiza kikamilifu, kwa ukamilifu na kwa haki majukumu makubwa ya nafasi yangu kama Rais wa Jamhuri ya Madagascar. huku akiapa  kwamba atatekeleza mamlaka niliyopewa na nitatoa nguvu zangu zote kulinda na kuimarisha umoja wa kitaifa na haki za binadamu."

Awali, Randrianirina alitangaza kuwa jeshi limechukua madaraka na kuvunja taasisi zote isipokuwa Bunge la Kitaifa. Alieleza kuwa kamati inayoongozwa na jeshi itatawala kwa kipindi cha hadi miaka miwili sambamba na serikali ya mpito, kabla ya kuandaa uchaguzi mpya.

Randrianirina alikuwa kamanda wa kikosi maalum cha CAPSAT, ambacho kilihusika katika mapinduzi ya mwaka 2009 yaliyomleta Andry Rajoelina madarakani. Hata hivyo, wiki iliyopita alijitenga na Rajoelina, akiwahimiza wanajeshi wasiwafyatulie risasi waandamanaji.

Wakati vijana wengi wakishangilia kuanguka kwa utawala wa Rajoelina, baadhi yao wameanza kuonyesha wasiwasi kuhusu kasi ya jeshi katika kujaza nafasi ya uongozi.

Rajoelina, ambaye alikimbilia nje ya nchi mwishoni mwa wiki, aliondolewa madarakani na wabunge, lakini amekataa kujiuzulu licha ya maafisa wengi wa usalama kujiondoa upande wake.