Jumatano , 21st Aug , 2019

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo, amewaagiza Wakurugenzi hadi kufikia Desemba 2019, kuhakikisha wale walimu wote waliosomea elimu yenye mahitaji maalumu, wanawahamisha na kuwapeleka katika shule zenye mahitaji maalumu na jumuishi.

Waziri Jafo amebainsha hayo Agosti 21, akizungumza na Maafisa Elimu kutoka mikoa yote 26, na kuwaagiza Maafisa Elimu kudumisha upendo kwa watoto wenye mahitaji maalumu kwani wanahitaji upendo wa hali ya juu.

"Ifikapo Disemba 2019 walimu wote waliosomea elimu yenye mahitaji maalumu,  wahamishiwe kwenye shule zenye mahitaji maalumu, ama shule jumuishi na wahakikishe walimu hao wote walipwe posho zao zilizokamilika, hatutaki kurundika madeni katika suala zima la uhamisho wa walimu" amesema Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo amebainisha namna watoto wenye mahitaji maalumu wanavyokumbana na mazingira magumu mashuleni, na kuwaagiza maafisa elimu maalumu kutembelea katika shule hizo, ili kubaini changamoto wanazokumbana nazo walemavu.

"Watoto wanadharirika watoto wanapata shida hata wewe msimamizi mkuu hujawahi fika eneo lile, utamshauri nini Mkurugenzi kama hata wewe unashindwa kutembelea eneo lako, nilifika pale shule  ya uhuru Mchanganyiko, nilifika pale maeneo yao hadi nilitoa machozi, nilifika Shule ya Mafinga  nilimkuta mtoto mlemavu hataki hata kwenda chooni kwa sababu choo chenyewe kilikuwa kibovu hadi wadudu wanatoka" amesema Waziri Jaffo.