Jumatano , 25th Mar , 2020

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, leo amekataa kuzungumzia wala kujibu maswali yaliyokuwa yakihoji kuhusu ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona na kwamba leo ilikuwa ni nafasi ya kuzungumzia masuala ya rasilimali watu katika sekta ya afya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amekataa hii leo Machi 25, 2020, Jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya nafasi 1,000 za ajira kwa madaktari zilizotolewa na Serikali, lengo likiwa ni kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

"Leo sitaki kuongea habari ya Corona, mjiandae kesho tunaweza kukutana hapa saa 2:30 asubuhi, kwa sababu tusiharibu kikao hiki muhimu cha kuzungumzia rasilimali watu katika sekta ya afya ili kuweza kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za afya, bado wananchi wanaenda kwenye vituo vya afya wana Malaria, TB, HIV, Kisukari, Moyo na Saratani, Corona tutaongea kesho" amesema Waziri Ummy. 

Mpaka sasa idadi ya wagonjwa waliothibitika kuathirika na ugonjwa hatari wa mapafu na mafua makali, unaosababishwa na Virusi vya Corona hapa nchini ni 12.