Alhamisi , 7th Aug , 2014

Kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania LHRC kimesema ni vyema Bunge Maalumu la Katiba likasitisha vikao vyake kutokana na kufanyika mabadiliko ya kanuni ambayo yatapelekea kupatikana kwa Katiba ambayo haina ridhaa ya wananchi.

Mkurugenzi mkuu wa kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC Dkt Hellen Kijo-Bisimba.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa kituo hicho Dk. Hellen Kijo-Bisimba amesema kumekuwepo kwa kauli za baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na wajumbe wa bunge maalumu, zinazoashiria mwelekeo mbaya wa kukiuka misingi ya kidemokrasia na utawala wa kisheria.

Aidha, Dk. Bisimba ameongeza kuwa kituo hicho kimesikitishwa na kupinga vikali kauli ya Mweyekiti wa Bunge la Katiba kutoa maelekezo kwa serikali ya Tanzania kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza midahalo inayohusu Katiba ambapo amesema matamko hayo yana lengo la kuwazuia watanzania kupata habari na taarifa juu ya mwenendo wa uboreshaji wa maoni yao yaliyopo kwenye rasimu na kujua hatma ya mchakato wa Katiba mpya.

Aidha katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoani Arusha inawashikili kwa mahojiano wanne baada ya kubainika kuwa na uhusiano ya karibu na baadhi ya watuhumiwa wa kesi za ugaidi ambao kesi yao imeanza kusikilizwa jijini humo.

Akizungumza leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha SACP Liberatus Sabas, amesema watu hao wamekamatwa baada ya kufanyiwa upekuzi nyumbani kuwa ni Adam Mussa anayejulikana jina maarufu Pakasi, mkazi wa Siwandeti, Wilayani Arumeru na kukutwa bunduki ya kienyeji ikiwa na risasi 38 pamoja na bunduki aina ya Shortgun.

Kamanda Sabas mesema pia wanashikilia watu wengine watatu na baada ya kuwahoji wamebaini wana mahusiano ya karibu na watuhumiwa wa ugaidi wa kulipua mabomu na kumwagia watu tindikali, ambao wapo mahakamani.

Kamanda Sabas amesema mara baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa huo watatu watafikishwa mahakamani, kujibu shitaka linalowakabili ambapo Oparesheni ya kuwakamata watuhumiwa zaidi wa matukio hayo inaendelea.