Jumatano , 22nd Mei , 2019

Jumla ya watuhumiwa 17 wa makosa mbalimbali waliokuwa wamehifadhiwa kwenye ukumbi wa jengo jipya la Mahakama ya Mkoa wa Geita kusubiri mashauri yao kutajwa mahakamani, wametoroka katika mazingira ya kutatanisha.

Askari wa Jeshi la Polisi

Awali Mahabusu hao walikuwa wamehifadhiwa katika Ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita kabla ya kuhamishiwa katika ukumbi wa jengo jipya la mahakama hiyo linaloendelea kujengwa ili kupisha kikao cha Mahakama Kuu kinachoendelea mbele ya Jaji Ismail.

Mkuu wa Mashitaka, Ofisi ya Mashitaka Mkoa wa Geita, Bibiana Kileo, ameeleza  kuwa mahabusu waliotoroka hawahusiani na kikao cha Mahakama Kuu kilichoanza mei 20 hadi Juni 16 mbele ya Mhe. Jaji Ismail kwa ajili ya kusikiliza na kutolea maamuzi kesi za mauaji.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Robert Rumanyika amesema Jeshi hilo halijaanza utaratibu wa kupeleka mahabusu mahakamani kama ilivyo kwa baadhi ya Mikoa hapa nchini na kwamba tukio la kutoroka kwa mahabusu hao haliko chini yake.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, akizungumza kwa sharti la kutokupigwa picha, amesema asingependa kuzungumzia tukio hilo kwa sasa kwa hofu ya kuvuruga upelelezi.

Tazama hapa chini.