Jumanne , 18th Aug , 2015

Mgombea Urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Mh Edward Lowasa amekamilisha ziara ya kutafuta wadhamini katika visiwa vya Zanzibar na amewaahidi wananchi wa visiwa hivyo kutumia uwezo wake wote kushughulikia kero.

Mgombea Urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Mh. Edward Lowasa

Akizungumza na wananchi hao katika viwanja vya Kibanda Maiti visiwani Zanzibar Lowassa amesema hatua iliyofikia sasa suala la kuiondoa CCM, madarakani halina mjadala kilichobaki ni utekelezaji ambao asilimia kubwa uko mikononi mwa wananchi.

Lowassa amesema kuwa yeye ni muumini wa serikali tatu toka mwaka 1990 walipounda kundi la G55 likiwa na harakati za kuwakomboa watanzania hivyo muda ukifika ataeleza msimamo wake juu ya serikali tatu.

Aidha ameongeza kuwa kama atapewa ridhaa ya watanzania ataweza kuwashughulikia mashekh wa kikundi cha UAMSHO, ambao wanashikiliwa kwa tuhuma za ugaidi kwa hivyo haki itatendeka dhidi yao.

Awali makamu wa kwanza wa Rais Seif Sharifu Hamad na mgombea mwenza Juma Duni Haji na mwenyekiti wa CHADEMA, Mh Freeman Mbowe pamoja na kuelezea adhma ya UKAWA, ya kulinda na kudumisha muungano wameitaka serikali iliyoko madarakani kuacha kuwatisha watendaji hasa wa vyombo vya dola kuwa wakiingia madarakani watapoteza ajira zao.