Alhamisi , 6th Dec , 2018

Kesi inayowakabili viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Freeman Mbowe imesogezwa mbele tena hadi Disemba 21 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.

Jopo la viongozi CHADEMA, wakiwa kwenye kizimba vya mahakama.

Kesi hiyo ya msingi ambayo ilipangwa kusikilizwa leo na Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri lakini ilishindikana kutokana na kuwepo kwa kesi kwenye mahakama ya rufaa juu ya kupewa au kutopewa dhamana kwa Freeman Mbowe pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko.

Akizungumza mara baada ya kutoka kwenye shauri hilo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Vicent Mashinji amesema "tutarudi tena tarehe 21, kwa ajili kuja kutajwa tena kesi yetu halafu itategemea kama itakuwa imeshatoka kwenye mahakama rufaa nchini."

Waliokuwa mahakamani hapo walishuhudia kuimarishwa kwa hali ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha hakutokei vurugu na hali ya sintofahamu wakati kesi hiyo ikiwa inaendelea.

Viongozi wengine wako nje kwa dhamana lakini Mbowe na Esther Matiko wamerudisha mahabusu baada ya kufutiwa dhamana na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kujiridhisha viongozi hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Mbowe na viongozi wengine wa CHADEMA wanashtakiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji nchini NIT Akwilina Akwilini.