Jumatatu , 14th Aug , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora wawapeleke watoto wao shule na waache kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.

“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari.

“Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.

Aidha Waziri Mkuu amewaasa sana vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30. Pamoja na wazazi wanaooza mabinti zao ili wapate mahari, kwani  nao pia watakuwa kwenye hatari ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika kushirikiana na waoaji.