Alhamisi , 22nd Apr , 2021

Aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema kuwa upinzania kuminywa au kutominywa ni mtazamo tu ambao unaweza ukatumika kama nafasi ya kufanya vizuri zaidi au pia ukatumika vinginevyo.

David Kafulila.

Kafulila amesema hayo leo alipokuwa akijibu swali la mtangazaji Samson Charles ambaye ni Mtaalam wa Siasa ndani ya kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio, kuhusu mtazamo wake kama kweli upinzani uliwahi kuminywa.

''Kuhusu upinzani bungeni nadhani bado nchi inahitaji upinzani imara ili kuendelea kuchagizana kwenye mijadala muhimu ya kitaifa, na kuhusu kuminywa kwa upinzani nadhani kila kitu ni nafasi unaweza ukaminywa kumbe ndio umepewa nafasi nyingine,'' alijibu David Kafulila.

Aidha, Kafulila amependekeza pia baada ya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo Aprili 22, 2021 bungeni, basi lianze kuoneshwa mubashara kupitia televisheni ili wananchi wawapime wabunge wao.

''Baada ya hotuba ya Rais leo nadhani sasa kuna haja bunge liwe live (mubashara) ili hata wananchi wanavyojadili wawe wanaona mchango na maoni ya wabunge wao na kama itakuwa hivyo, kila mbunge atajituma kwasababu wananchi watamuona na kumpima,'' amesema Kafulila.