Alhamisi , 22nd Sep , 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mataifa ulimwenguni kuungana katika kutoa mchango kwa mfuko wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).

Makamu wa Rais Tanzania Dkt. Phillip Mpango

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akihutubia mkutano wa saba wa kuwezesha mfuko wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund) uliofanyika New York nchini Marekani.

Dkt. Mpango amesema migogoro ya sasa ya kimataifa imepunguza juhudi za kurejesha uchumi wa nchi nyingi ulioathirika na janga la UVIKO19 na kuongeza changamoto mpya katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu hivyo hakuna budi wote kwa pamoja kuona haja ya kuunga mkono kazi nzuri ya mfuko huo wa Kimataifa ili kuendeleza mafanikio katika kukabiliana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Global Fund, ambao umekuwa na matokeo chanya yaliopelekea kupunguza idadi ya vifo kwa magonjwa ya Ukimwi ,Kifua Kikuu na Malaria huku akiishukuru Bodi ya Global Fund kwa kuinga mkono Tanzania kwa miaka mingi.

Leo Septemba 22, 2022 Makamu wa Rais anatarajia kuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.