Jumatano , 9th Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda, amezindua mfumo wa kuwawezesha wananchi wa mkoa huo, kuwasilisha kero na changamoto walizonazo kwa kutumia simu ya mkononi na ujumbe wao kuwafikia watendaji kwa haraka.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam

Mfumo huo ameuzindua leo Oktoba 9, 2019, wenye mlengo wa kuwabaini watendaji wasiotekeleza majukumu yao, mfumo ambao unauwezo wa kutoa majibu ndani ya muda mfupi, jambo litakalosaidia kuokoa muda na gharama.

''Nimeamua kuanzisha mfumo huu, baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye ofisi za umma na kupewa majibu ya njoo kesho, pasipokujua kuwa wamepoteza muda na nauli zao kufuata huduma'' amesema Makonda.

Aidha Makonda amewahimiza wananchi, kutumia mfumo huo kueleza kero zote zinazowakabili, ikiwemo Afya, Barabara, Elimu, Maji, Umeme pamoja na miradi inayokwama na kutoa taarifa pindi wanapobaini uhalifu kwenye mtaa.