Jumanne , 21st Jun , 2016

Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imebaini uwepo wa wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuuza bidhaa zao ndani ya magari wanayoyaegesha maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, kitendo kinachoikosesha manispaa hiyo mapato.

Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Faith Shaibu

Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala Bi. Tabu Shaibu, amesema hayo katika mahojiano na EATV iliyotaka kufahamu juhudi zinazochukuliwa na manispaa hiyo hasa kupitia zoezi linaloendelea hivi sasa la kukusanya mapato kutoka kwa wadaiwa sugu.

“Kupitia zoezi la wadaiwa sugu tumebaini mambo kadhaa na hasa namna baadhi ya watu wasioitakia mema Manispaa wanavyokwepa kodi kupitia mbinu mpya,” amesema Bi. Tabu Shaibu.

Amesema “Wanachokifanya ni kuweka bidhaa zao katika magari na kisha kuuza kupitia milango ya nyuma ya magari hayo ili iwe rahisi kwao kukimbia pindi wanapobaini kuwa kuna mamlaka inawafuatilia,”.

Amefafanua kuwa kutokana na kubaini mbinu hiyo, hivi sasa wamejipanga kuandaa utaratibu utakaowawezesha kukusanya ushuru na kodi kutoka kwa kundi hili la wafanyabiashara ambao usipofuatilia kwa makini unaweza kudhani kuwa ni biashara halali.

Kuhusu ukusanyaji mapato kutoka kwa wadaiwa sugu; Tabu amesema takribani shilingi bilioni mbili zimekusanywa katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita na hapa anaeleza changamoto inayowakabili katika zoezi hilo.

“Tuna vyanzo vingi vya mapato kama vile kodi za majengo, ushuru wa matangazo, malipo ya vibali na leseni pamoja na tozo mbali mbali ambazo wahusika wamekuwa wakaidi kulipa kwa wakati, hivi sasa tunaendesha zoezi la ukusanyaji mapato hayo kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha,” amesema Afisa Uhusiano huyo wa Manispaa ya Ilala.

Amesema Uongozi wa Manispaa unakusudia kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote sugu, uamuzi ambao hata hivyo amesema sio vema kufikia hatua hiyo kwani lengo la manispaa ni kuweka mazingira mazuri ya ushirikiano na wateja wake na sio kukomoana.

“Si vema na wala sio nia ya manispaa kuwafikisha wateja wake mbele ya vyombo vya sheria, tunapenda kuwasihi wadaiwa wahakikishe wanalipa madeni yao kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kuepuka adha ya kufikishwa mahakamani,” amefafanua Bi. Tabu.