Alhamisi , 25th Jun , 2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoani Manyara inawashikilia Mwenyekiti wa CCM tawi la Maisaka Kati wilayani Babati na katibu wa tawi hilo kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa.

Chama cha Mapinduzi CCM

Mwenyekiti wa tawi hilo, Bakari Khatibu na Katibu wake, Juma Swalehe wanatuhumiwa kwa kuomba na kupokea rushwa ya Shilingi laki mbili (200,000), kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya TAKUKURU Na. 11 ya mwaka 2007.

Wawili hao waliomba na kupokea rushwa hiyo kutoka kwa Muinjilisti wa Kanisa la Kilutheri la Komoto kwa maelezo kuwa baada ya kupokea fedha hizo wangemuachia kiwanja walichokuwa wakidai kuwa ni mali ya CCM.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Makungu amesema kuwa hawatasita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa aina hiyo ambayo wana uhaba wa maarifa na wanaodhani kuwa hawawezi kuguswa kwakuwa ni waajiri wa chama tawala.

"Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote, wana haki ya kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria bila kuzingatia utaifa, kabila, wanapotokea, maoni yao ya kisiasa, dini, jinsia au hali yao ya maisha", amesema.