Jumatatu , 26th Mei , 2014

Mapigano baina ya wakulima na wafugaji yamezuka upya katika wilaya ya Kilindi, ambapo serikali imeombwa kuingilia kati mapema.

maeneo ya wafugaji wilayani Kilindi

Serikali imeombwa kuingilia kati haraka tatizo la kugombea mipaka kufuatia kuibuka kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji wa vijiji vitatu vilivyopo kata za Tunguli na Kwekivu wilayani Kilindi.

Wakizuungumza na EATV katika kijiji cha Lusane kilichopo kata ya Tunguli wilayani kilindi viongozi wa madhehebu ya dini na wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wamedai kuwa baadhi ya makundi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wakulima yamekuwa yakiingia na silaha za moto na baridi kwa lengo la kuwadhuru baadhi ya wafugaji baada ya mwenzao mmoja kuchomwa na mshale sehemu za ubavuni hatua iliyoanza kuwapa hofu ya kuibuka kwa mapigano.

Kwa mujibu wa kiongozi wa dhehebu la kanisa la kilutheri usharika wa Lusane mchungaji Malaki Ole Tunuo amemweleza mkuu wa wilaya ya Kilindi kuwa migogoro hiyo imeshamiri zaidi katika vijiji vya Lusane kilichopo kata ya Tunguli na vile vya Kitingi na mtolo vilivyopo kata ya Kwekivu kufuatia viongozi wa serikali ngazi za vijiji na kata kuuza maeneo yote wafugaji na kusababisha jamii hiyo kuhangaika na mifugo yao kutafuta maeneo ya malisho.

Kwa upande wake mzee wa kimila wa kijiji cha Lusane Bwana Emmanuel Sing'ati amesema makundi hayo yamekuwa yakitembea na silaha za moto na baridi ikiwemo bunduki,mishale na mapanga kuwatafuta baadhi ya wafugaji hatua ambayo imekuwa ikiwapa hofu ya kuibuka mapigano baina ya pande hizo hizo mbili hivyo wamesisitiza kuwa ni vyema serikali ikaharakisha zoezi la kumega mipaka ya vijiji hivyo ili kuepuka madhara ya vurugu hizo.

Kufuatia hatua hiyo mkuu wa wilaya ya kilindi Bwana Selemani Liwowa akizungumza na makundi ya wafugaji wa vijiji vitatu vya Lusane, Kitingi na Mtolo amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilindi kuhakikisha kuwa wanaanza mara moja zoezi la kugawa mipaka baina ya kijiji kimoja kwenda kingine ili kuepuka madhara zaidi ya kugombea maeneo ndani ya vijiji vyao.