Ijumaa , 18th Jan , 2019

Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Hai linaloongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Bi Irene Lema amekanusha taarifa ya kupokonywa ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo kama ilivyotangazwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya hivi karibuni.

Mbunge wa Jimbo la Hai Freeman Mbowe

Kwa mujibu wa Katibu huyo Freeman wa Mbowe, hawajawahi kutumia ofisi yeyote iliyopo ndani ya Halmashauri ya Hai kutokana na Freeman Mbowe kuwa na wageni wengi huku chumba cha halmashuri kikishindwa kuhudumia idadi ya wageni wengi aliyokuwa nao.

Irene Lema amesema, "Mbunge hana ofisi ndani ya Halmashauri ya Hai, na aliamua kuweka nje ya halmashauri kwa sababu ilikuwa ni ndogo sana na akaamua kuweka nje ili kuwapokea wageni wengi wanatokea ndani na nje ya jimbo, hatujawahi kuitumia ofisi ambayo Mkuu wa Wilaya amesema amempokonya Mbunge."

"Ofisi yetu iko wazi muda wote na ninavyokwambia muda huu nimetoka kukutana na watu watatu ambao wanashida na Mbunge, kwa hiyo ofisi yetu tunashirikiana vizuri sana na wafanyakazi wote wa halmashauri ya Hai akiwemo Mkurugenzi tena bila kujali vyama vyao", ameongeza Irene Lema.

Mapema wiki iliyopita hii, Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya alitangaza kumpokonya Freeman Mbowe ofisi yake, akidai kuwa kiongozi huyo hajaonekana katika ofisi yake kwa muda mrefu.