Meya CHADEMA azikataa milioni 200 za CCM

Jumamosi , 17th Nov , 2018

Meya wa Manispaa ya Iringa Mjini Alex Kimbe, amefunguka kuwa amekuwa akijikuta na kesi mbalimbali mahakamani kwa kile alichokidai kuwa ni hujuma anazofanyiwa na Chama Cha Mapinduzi, kwa kuwa amekataa kuhamia ndani ya chama hicho.

Meya wa Manispaa ya Iringa Mjini Alex Kimbe,.

Mapema jana asubuhi kulianza kusambaa kwa taarifa kuwa Meya huyo wa Iringa Mjini, alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),  kwa madai ya kukutwa na fedha ya mtego zaidi ya shilingi milioni 2 na mzabuni Nancy Nyarusi.

Akizungumza Mjini Iringa Kimbe amesema “hii si mara ya kwanza kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali na wote wanaonishtaki ni makada wa Chama Cha Mapinduzi.”

Lengo la CCM ilikuwa ni kupata Meya anayetokana na Chama Cha Mapinduzi na walipoleta hoja hiyo ikashindikana kwa sababu walikiuka kanuni, na baada ya kufeli wakaamua kuniundia tuhuma mbalimbali.” Amesema Kimbe

Wanafanya yote hayo ili nikubali milioni 200, nijiunge nao na mara ya mwisho walinifuata baadhi ya viongozi wa CCM ili wanipatie hizo fedha na wanifutie kesi, na huu msimamo wangu ndiyo chanzo kikubwa haya yote.”  Ameongeza Meya huyo.