Alhamisi , 14th Apr , 2016

Licha ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kunufaisha sekta mbalimbali hapa nchini zikiwemo sekta za Elimu, Afya pamoja na Ujasiriamali mfumo huo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Hospitali ya Tumbi ni moja kati ya Hospitali zinazofaidika na mfumo wa TEHAMA

Changamoto hizo zimetolewa mkoani Morogoro kwenye mkutano wa wadau wa (ICT), wakijadili maendeleo ya mradi wa utawala bora na ujasiriamali kupitia tafiti, elimu na Tehama, mradi huo unakabiliwa na changamoto za ukosefu wa wataalamu pamoja na katizo la umeme la mara kwa mara hali inayosababisha kudorola kwa ukuaji wa teknolojia nchini.

Wadau hao wamesema mbali na mradi huo kuwa na changamoto nyingi lakini hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro pamoja na hospitali ya rufaa mkoa wa Pwani ni moja ya maeneo yaliyoanza kunufaika na mradi huo.

Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambao ndio wanufaika wakubwa wateknolojia hiyo wamesema kulikuwa na tatizo la upatikanaji wa vitabu lakini kutokana na teknolojia ya Tehama sasa wanaweza kuwasiliana na kusoma vitabu katoka vyuo vingine kupitia mfumo huo.

Hata hivyo baadhi ya wadao wamesema kukosekana kwa mfumo wa mawasiliano katika hospitali nyingi hapa nchini kumekuwa kukisababisha upotevu mkubwa wa dawa hospitalini.

Aidha, wamesema kuwa kukosekana kwa mfumo huo kumechangia watu wengine wakipotelewa na miili ya ndugu zao ambapo wamesema endapo serikali itaunga mkono jitihada za wadau katika kukuza teknolojia kutasaidia hospitali hizo kutunza kumbukumbu muhimu mbalimbali.