Jumamosi , 24th Oct , 2020

Ikiwa zimebaki siku tatu kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Tanzania,wanawake viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa wamekemea vikali vitendo vya uvunjifu wa amani kwa wale wote wenye nia ovu ya kutaka kuvuruga Uchaguzi huo.

Waziri wa Nchi, Sera,Bunge,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu,Jenista Mhagama

Wakizungumza hii leo katika mkutano na waandishi wa habari,kupitia Katibu Mtendaji Anna Ryoba Paul, wanawake viongozi  wamelipongeza jeshi la polisi kwa jitihada zake za kulinda amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.

'' Pia tunawataka viongozi wa siasa kutotumia viongozi wa dini katika siasa ili kuepusha mgawanyiko miongoni mwa wananchi ''Alisema katibu huyo Anna Paul

Naye Waziri wa Nchi, Sera,Bunge,Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu,Jenista Mhagama, ameungana na viongozi hao kwa kuzungumza nao kwa njia ya simu katika mkutano huo na kusema kuwa hatua hiyo ni nzuri  kwa nafasi walionayo na ni jukumu lao kulinda na kudumisha amani ya nchi yao.

''Kukutana kwenu kuna umuhimu katika kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi mnaowataka na mna jukumu kubwa la kuhamasisha na kuilinda amani ya nchi.''Mh. Jenista aliongeza

Aidha Mh. Jenista amesema kuwa waathirika wakubwa iwapo amani na utulivu vitatoweka ni wanawake  na  kuwaasa watu wote kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi hivyo ni muhimu kuilinda amani ya nchi na siku ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi.