Jumanne , 15th Jul , 2014

Migogoro ya ardhi nchini Tanzania imetajwa kuchukua asilimia 41 kati ya migogoro mbalimbali katika maeneo mengi nchini na kusababisha vifo na mamilioni ya mali kupotea.

Mkurugenzi wa Idara ya Maboresho na Ushawishi wa kituo cha Sheria na haki za Banadamu LHRC Bw. Harold Sungusia.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Maboresho na Ushawishi wa kituo cha Sheria na haki za Banadamu LHRC Bw. Harold Sungusia na kuongeza kuwa chanzo cha tatizo hilo ni ununuzi wa ardhi kiholela pasipo na utaratibu wa kisheria pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Aidha Bw. Sungusia ameitaka Serikali ichukue hatua za dharura katika kutatua migogoro ya ardhi iliyopo na kuongeza kuwa ni vyema elimu ikatolewa kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi ili kuondoa tatizo hilo katika kuitafsiri sheria.

“Wengi wa wajumbe wa mabaraza ya kata hawana mafunzo ya kutosha kuhusu sheria ya ardhi na matokeo yake wengi wanafanya kitu ambacho hawakijui na hivyo wanajaribu kutatua tatizo kwa kusababisha tatizo kubwa kuliko la awali”

Hata hivyo amaesema ni vyema mifumo katika ngazi ya kata, wilaya, mahakama na Wizara kushirikiana kwa pamoja katika kutoa maamuzi katika migogoro ya ardhi nchini.