Ijumaa , 21st Nov , 2014

Ukosefu wa elimu ya uzazi na elimu ya uzazi wa mpango bado ni changamoto kubwa kwa wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,hali ambayo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa mimba za utotoni kwa kiasi kikubwa.

Aliekua Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Ally N. Rufunga akiongea na wakazi wa Kishapu.

Mratibu msaidizi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto wa wilaya ya kishapu Bi. Suzana Kulindwa ameyabainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema idadi kubwa ya wasichana ambao wanabeba mimba kuanzia miaka 14 hadi 19.

Amesema kuwa kwa mwaka 2013 wanawake 13,373 walihudhuria kliniki na kati yao 2,562 walikuwa na umri wa chini ya miaka 20 ikiwa ni sawa na asilimia 19.1 na kuwa katika kipindi cha Januari na Juni mwaka huu wanawake 1,370 wenye umri wa chini ya miaka 20 walihudhuria Kliniki sawa na asilimia19.9 wakiwa wajawazito.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2014, kati ya wanawake 6,871 waliohudhulia 1,370 , wamebainika ni vijana waliokuwa na umri wa chini ya miaka 20, hali aliyodai imekuwa ikisababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na uzazi.