
Mkutano huo wa siku mbili ulioanza jana mjini The Hague Uholanzi, uliwakutanisha viongozi wa nchi wanachama wa NATO ambao walijadiliana kuhusu suala la kuongeza matumizi yao ya ulinzi, namna ya kuimarisha muungano huo pamoja na mizozo inayoendelea duniani ikiwa ni pamoja na ile ya Mashariki ya Kati na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alihutubia bunge la Uholanzi akituma pia ujumbe kwa viongozi wa NATO kuwa Urusi bado ni kitisho kwa kuwa imekuwa ikiunda ushirikiano na tawala za kikatili akisisitiza kuwa kutokana na msaada wa Iran, Moscow iliishambulia nchi yake kwa droni takriban 29,000 aina ya Shaheed, akisisitiza kuwa wasingelikuwa na uwezo wa kuzuia mashambulizi hayo bila ya msaada wa washirika wake wa Magharibi.
Uingereza kwa upande wake imerejelea kauli yake ya kuongeza pia matumizi yake ya ulinzi hadi kufikia asilimia 5 ya Pato la Taifa na kwamba itarejesha tena ndege za kivita chapa F-35A maarufu kama "Lockheed Martin" zenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia ili kutanua safu ya silaha ya nchi hiyo na kuimarisha jeshi la NATO . Kwa sasa Uingereza inayo makombora ya kurushwa kutoka chini ya bahari.
Katika taarifa, waziri Mkuu Keir Starmer amesema hatua hii ambayo ni ya kwanza tangu kumalizika kwa enzi za vita baridi inachukuliwa kwa kuzingatia nyakati za sasa zisizotabirika na zinazohitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya usalama hasa kutokana na kitisho cha Urusi na Marekani kuonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa Ulaya.